Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Abdul-Sayed, ambaye ni daktari na mwanaharakati anayetetea mabadiliko ya kijamii yenye mwelekeo wa maendeleo, ameandika historia baada ya kushinda katika kinyang’anyiro kilichokuwa na ushindani mkali wa nafasi ya useneta wa Marekani katika jimbo la Michigan. Amemshinda mgombea wa chama cha Republican, Mike Rogers, na kuwa seneta wa kwanza Muislamu katika historia ya nchi hiyo.
Ushindi wa Abdul-Sayed ulipatikana baada ya chama hicho kupata udhibiti wa Baraza la Seneti siku ya Jumanne, kufuatia ushindi wa kushtukiza katika majimbo ya Texas, Kansas na South Carolina.
Abdul-Sayed alitangaza ushindi wake katika kinyang’anyiro cha nafasi ya useneta wa Marekani katika jimbo la Michigan mapema siku ya Jumatano, akiwa katika makao makuu ya chama cha Democratic cha jimbo hilo jijini Detroit.
Katika hotuba yake ya usiku wa uchaguzi, aliwaambia wananchi waliokuwa wamekusanyika hapo: «Mliweka matumaini yenu kwa mgombea ambaye wengi hawakutarajia angeweza kushinda. Mlinipokea katika nyumba zenu, makanisa yenu na masinagogi yenu.»
Alisifu vuguvugu lililojengeka katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa kampeni zake za uchaguzi katika miji mikubwa na midogo zaidi ya jimbo la Michigan. Alisema kuwa wapiga kura walimpa nguvu katika nyakati ngumu zaidi alizopitia.
Mpinzani wake na watu waliompinga, akiwemo Donald Trump na makamu wake wa rais, J. D. Vance, waliongoza kampeni iliyokuwa kwa kiasi kikubwa imejengwa juu ya chuki dhidi ya Uislamu. Mara nyingi walikuwa wakitaja jina lake na imani yake ya Kiislamu, miongoni mwa kauli hizo ni ile ya Rais Trump, ambaye alimwita «Mujahidina» na kudai kuwa anapaswa kupita kwenye mashine ya ukaguzi wa vyuma kabla ya kuruhusiwa kuingia katika Baraza la Seneti.
Abdul-Sayed alisema kuwa wakosoaji wake, badala ya kujadili masuala yanayowagusa wananchi kama vile gharama za mafuta na vyakula, wameamua kuchochea migawanyiko, kwa sababu hawana majibu ya matatizo ambayo, kwa mujibu wake, wao wenyewe ndio wamesababisha.
Chanzo: Shirika la Habari la The Guardian.
Maoni yako